Mekatilili Wa Menza

Mekatilili Wa Menza (au Makatilili, yaani Mama Katilili) alikuwa mwanamke wa Kenya aliyewaongoza Wagiryama dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza na sera kikamilifu katika mwaka wa 1913 hadi 1914.

Wagiriama ni watu wa kabila moja katika kundi la makabila tisa (Mijikenda) ambao hukaa pwani ya Kenya; walikuwa na maskani takatifu sehemu ziitwazo Kaya, ambazo zilipatikana katika maeneo ya misitu, mojawapo ambayo iliharibiwa kwa kulipuliwa na utawala wa kikoloni wa Uingereza mwaka wa 1914. Hii ilikuwa Kaya Fungo.

Mekatilili alizaliwa katika miaka ya 1860 huko Bamba katika kaunti ya Kilifi. Alikuwa binti pekee katika familia ya watoto watano. Kaka yake mmoja alitekwa nyara na Waarabu wafanyabiashara ya utumwa na hakuwahi kuonekana tena.

Mekatilili alipinga utawala wa kikoloni kutokana na sababu za kiuchumi na kijamii. Hakutaka Wagiriama kuajiriwa na serikali ya kikoloni maana alitaka wabaki nyumbani mwao waifae jamii. Pia aliona kuwa mila na desturi za Mwingereza zilikuwa zikiingilia mila na desturi za Wagiriama, jambo lililomhuzunisha.

Mekatilili alitekwa na Waingereza na kupelekwa uhamishoni Mumias katika Mkoa wa Magharibi wa Kenya. Kulingana na rekodi za ukoloni wa Uingereza, alirejea katika eneo lake la uraia miaka mitano baadaye ambapo aliendelea kupinga kulazimishwa kwa sera na amri za kikoloni.

Alifariki mwaka wa 1924 akazikwa Bungale, katika Jimbo la Magarini.


From Wikipedia, the free encyclopedia ยท View on Wikipedia

Developed by Tubidy